WAZIRI MHAGAMA: SERIKALI KUANZA UJENZI WA MAJENGO MAPYA BOMBO.
Posted on: February 22nd, 2025
Waziri wa Afya Mheshimiwa Jenista Mhagama leo Februari 22, 2025 ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo katika ziara yake ya kikazi Mkoani humo kufuatia ujio wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzia kesho Februari 23,2025 huku ikitarajiwa kutamatika tarehe 02, Machi 2025.
Kupitia ziara hiyo Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuanza ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo kwa kuanza na Jengo la Wodi ya Mama na Mtoto kabla ya mwezi wa tano ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Uzazi kwa mama na mtoto.
Amesema "Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia imeipa kipaumbele Sekta ya Afya ambapo zaidi ya trillioni 8 zimewekezwa katika kipindi hiki kifupi, na Mkoa wa Tanga ni moja ya Mikoa ilyofaidika na fedha hizi".
Aidha, Serikali inafanyia kazi changamoto ya majengo katika Hospitali ya Bombo ambapo kwa sasa ujenzi utaanza ili kubadilisha muonekano wa Hospitali hiyo na kuanza kwa ujenzi wa Jengo la Wodi ya wazazi ambalo litakua na huduma zote fungamanishi ikiwemo upasuaji pamoja na vipimo vya maabara.
"Kiu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha tunaendelea kupunguza vifo vya mama na mtoto, tumetoka kwenye idadi ya vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 hadi vifo 104 kwa vizazi hai 100,000, lakini tunatamani Hospitali yetu ya Bombo iendelee kuongoza katika kupunguza idadi ya vifo vya akina mama wakati wa kujifungua".
Waziri Mhagama ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wakazi wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kwa wingi kumpokea Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha uwezo wa kusimamia miundombinu ya utoaji wa huduma za tiba, "Afya ni maendeleo, Afya ni usalama wetu na Afya ndio ulinzi wa mkoa wetu wa Tanga,"
Pia, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo Dkt. Frank Shega ameiomba Serikali kuwezeshwa katika Ukarabati wa majengo katika Hospitali hiyo pamoja na kupatiwa fedha ili kujenga majengo mengine mapya kwa ajili ya kuongeza huduma na kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za afya kwa wananchi.