Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

MABADILIKO YA KIUONGOZI HOSPITALI YA RUFAA YA BOMBO NI KUBORESHA HUDUMA

Posted on: January 21st, 2024

Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali Watu wa Wizara ya Afya Bw. Daniel Temba amesema mabadiliko ya kiuongozi yaliyo fanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo ni kuhakikisha wanaboresha huduma na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Bw. Temba aliyasema hayo wakati wa halfa ya makabidhiano ya ofisi kwa Mganga Mfawidhi Mpya Dkt Frank Shega kutoka kwa aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt Naima Yusuf katika Hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo.

Pamoja na mabadiliko hayo wanampongeza Dkt Naima Yusuf kwa kipindi chake chote akiwa kiongozi mkuu wa hospitali kwa  kufanya kazi nae kwa karibu sana kuhakikisha wanaboresha huduma kwenye hospitali ambayo imekuwa ni tegemeo kubwa wananchi wa mkoa wa Tanga na maeneo jirani.

Aidha alisema kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu kwa kipindi cha muda mfupi imefanya maboresho makubwa sana kwenye sekta ya Afya katika maeneo ya miundombinu,vifaa tiba na watumishi, na vitu vyote hivyo vinalenga kutoa huduma ipasavyo kwa wateja,wagonjwa na  wananchi .

Alisema jambo hilo limekuwa likisimamiwa na Rais Dkt Samia Suluhu na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambaye amekuwa akipambana usiku na mchana  na viongozi wa wizara kufikiria kwamba kwa hayo yaliyofanyika mapinduzi ya kuboresha sekta hiyo wao kama watumishi wafanye nini, hivyo wote waliopo hapa wanadeni la kufanya kwa kutimiza wajibu wao kuwafikiishia wananchi huduma nzuri za Afya.

“Kupitia mabadiliko hayo tunategemea kila mmoja wetu ashirikiane na uongozi wa ndani na nje ya wizara kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na bora kwa watanzania,utaalamu wetu unategemewa na wananchi sana kuwapatia huduma bora za afya na sio suala la kuelekezwa “Alisema

Hata hivyo aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Tanga na viongozi wa CCM Mkoa kwa kuwa wamekuwa jicho la kuangalia mahitaji ya wananchi  yaweze kufikiwa kwa ubora unaotakiwa.

Awali akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo Mganga Mfawidhi mpya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo Dkt Frank Shega aliomba ushirikiano kwa sababu wanakwenda kufungua ukurasa mwingine wa kiutendaji wenye lengo la kuboresha huduma.

“Watumishi wenzangu nitafarijika sana kama nitapata mrejesho kutoka kwenu maana nguvu yangu ipo kwenu, mnaweza kufanya kazi yangu ya utendaji kuwa nzuri kama mikitimiza wajibu wenu na mimi nikitimiza wajibu wangu, pale panapohijika ushauri milango ipo wazi. Niwahaidi ushirikiano wa kutosha kabisa katika kutoa huduma kwa wananchi na kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao zote kwa wakati. Tukiwa na ushirikiano wa dhati kati ya Timu ya Viongozi wa Hospitali (RRHMT) na Timu ya Uongozi wa Afya Mkoa (RHMT) tutafikia malengo tuliyojiwekea kwa wakati. ” Alisema Dkt Shega

Naye kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo alisema Dkt Naima anayemaliza muda wake amefanya kazi kubwa sana kwa kujitahidi kubuni vitu mbalimbali ili kuhakikisha wanaongeza mapato kwenye Hospitali hiyo.