JAI TANGA WAENDESHA ZOEZI LA UCHANGIAJI DAMU HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA TANGA.
Posted on: August 13th, 2025
Taasisi ya Jamiiyatul Akhlakul Islamiyya (JAI) Mkoa wa Tanga mapema leo Agosti 13,2025 wameadhimisha Siku ya JAI kwa kuchangia Damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo ambapo wameungana na wadau kutoka kwenye Taasisi mbalimbali Jijini humo kuhakikisha wanatekeleza tendo hilo la huruma na baraka kwa kuchangia Damu inayokwenda kuwasaidia wenye uhitaji wakiwemo majeruhi wa ajali, wajawazito wakati wa upasuaji wa kujifungua, wenye seli mundu na wote wenye uhitaji wa damu.
Akitoa wito kwa jamii kuwa na utaratibu wa kuchangia damu Mwenyekiti wa JAI Tawi la Bombo Ostadh Mbwana Mbukuzi amesema jamii inatakiwa kuona umuhimu wa kujitokeza kuchangia damu pale huduma hiyo inapohitajika mahospitalini kwani kufanya hivyo husaidia kuokoa maisha ya mgonjwa anayehitaji damu pia ni thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu.
“Huu ni utaratibu wa kikundi chetu kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine, kwa hapa Bombo tumekuwa na utaratibu wa kuchangia damu mara kwa mara kwa kushirikisha na wadau wengine kutoka vyuoni na shule mbalimbali katika zoezi hili la uchangiaji damu.
JAI ni taasisi ya Kiislamu ambayo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali katika kuisaidia jamii kwenye mambo mbalimbali ikiwemo kusaidia matibabu kwa wasiojiweza, Uchangiaji damu na mazoezi mbalimbali yenye kuigusa jamii.