Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA TANGA WAIHAMASISHA JAMII KUCHANGIA DAMU

Posted on: August 20th, 2025



Jamii imetakiwa kufahamu kuwa ina wajibu wa kuchangia damu na kutambua umuhimu wa kushiriki zoezi hilo ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya damu kwa dharura ikiwemo kina mama wajawazito na majeruhi wa ajali licha ya kuwa zoezi hilo ni la hiari.

Rai hiyo imetolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Dkt. Frank Shega mapema leo Agosti 20, 2025 alipokuwa akiihamasisha jamii kuhusu zoezi la uchangiaji wa damu salama kupitia Kituo cha Habari cha Redio Maarifa cha Jijini Tanga.

"Kama tujuavyo, uhitaji wa damu ni wa dharura na kila mtu anapaswa kujua kuwa muda wowote yeye ni muhitaji wa damu kwa dharura, hivyo tuna wajibu wa kujitolea kuchangia damu ili kuwa na damu ya kutosha katika benki za damu jambo lililotusukuma kuiomba jamii kushiriki katika zoezi hili la hiari kwa wana Tanga tukiwa na lengo kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu wakati wote na kuongeza matumaini yao ya kuishi".

Aidha, Mteknolojia Maabara Hospitali ya Bombo Bw. Salvator Alexander, amewatoa hofu wale wanaoogopa kuchangia damu kuwa, kitendo hicho hakina madhara yotote kiafya kwa mchangiaji damu mwenye afya njema, na kuwataja watu wasiofaa kuchangia damu ni pamoja na wenye magonjwa ya kisukari, presha, watu waliofanyiwa upasuaji mkubwa karibuni na wale wanaotumia dawa za muda mfupi na mrefu kwa wakati huo.

“Zoezi la uchangaji damu ni zoezi la kitaifa ambalo limekuwa likiendelea kila siku,na jukumu letu kama watalamu ni kuihamasisha jamii kupitia vikundi na taasisi kujitoa kuchangia damu kwani hakuna kiwanda kinachoweza kutengezeza damu ya kumuongezea binadamu, bali ni binadamu pekee ndio wenye uwezo wa kuokoa maisha ya wagonjwa kwa kuchangia damu” amesema Bw. Salvator.

Ratiba zetu katika eneo la Uchangiaji Damu Jengo la Benki ya Damu ni kila siku za wiki kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi saa 2:30 asubuhi hadi 9:30 alasiri, tunawakaribisha vikundi,jamii au taasisi kuja kushiriki katika zoezi hili la uchangiaji damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya wenye uhitaji.