DC KUBECHA AZINDUA KISIMA CHA MAJI HOSPITALI YA BOMBO.
Posted on: February 19th, 2025
DC KUBECHA AZINDUA KISIMA CHA MAJI HOSPITALI YA BOMBO.
Mkuu wa wilaya ya Tanga Mjini Mheshimiwa Jafari Kubecha mapema leo Februari 19,2025 amezindua na kukabidhi kisima cha maji kwa Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo ili kupunguza adha ya upatikanaji wa maji Hospitalini hapo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo fupi ya kukabidhi kisima hicho kwa Uongozi wa Hospitali ya Bombo Mhe. Kubecha amesema pamoja na changamoto ambazo zipo katika baadhi ya maeneo Jijini Tanga lakini dhamira ya Serikali ni kuona maji yanapatikana katika kila kona ya nchi.
Aidha, Mhe. Kubecha amewaomba wadau wengi kujitokeza katika kuyatenda matendo haya ya imani ikiwemo kuisaidia Serikali katika kuhakikisha inasaidia jamii zao kwa kutoa sadaka zenye kuendelea kama kuchimba visima vya maji kwa lengo la kuwasaidia wananchi wenye uhitaji wa maji na badala yake kuacha kutumia fedha zao kwa ajili ya anasa.
Amesema kusudio la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan dhamira yake ni kuhakikisha maji yanasogezwa hadi kwa wananchi na kwa maeneo ambayo bado hakuna maji safi Serikali inaendelea kushughulikia kwa mipango ya muda mrefu na muda mfupi ikiwemo kuchimba visima na kuhakikisha jimbo la wananchi wa Jiji la Tanga wanafikia wastani wa kitaifa wa upatikanaji wa maji tofauti na ilivyo sasa.
Pia, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo Dkt. Frank Shega ameishukuru Serikali pamoja na mdau katika kufanikisha mradi huo wa Maji kupitia Taasisi isiyo ya kiserikali ya "Udugu Hazina Yetu" ambao umegharimu takribani shilingi milioni Tano unakwenda kuhudumia eneo kubwa la Hospitali hiyo katika shughuli za Maabara pamoja na kutunza bustani na kupunguza makali ya kulipa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ankara za Maji kwa matumizi ya Hospitali.