DC KALIMA: BODI YA USHAURI KASIMAMIENI MAJUKUMU YENU KWA UFASAHA NA WELEDI.
Posted on: July 25th, 2025
Rasmi leo Julai 25, 2025 Kaimu Mkuu wa Mkoa Mhe. Gilbert Kalima Mkuu wa Wilaya ya Mkinga amezindua Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ambapo wajumbe wa bodi wamehimizwa kuwa moja ya majukumu yao ni kushauri na kuwa kiunganishi kwa hospitali na jamii ili kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa katika hospitali kwa wananchi zinaendelea kuwa bora.
Akisoma hotuba hiyo Mgeni rasmi amesema “Kwa mchanganyiko wa ujuzi wa wajumbe mliopo katika Bodi hii, ni matumaini yangu kuwa pamoja na mambo mengine mtasimamia na kushauri vizuri matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo katika Hospitali, Hospitali kuzingatia vipaumbele katika utekelezaji wa utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi, kupokea na kujadili kwa umakini mkubwa taarifa za fedha za robo mwaka, nusu mwaka na zile za mwaka mzima pamoja na taarifa za utekelezaji wa huduma za Afya na kushauri namna nzuri ya upitishaji wa mikataba inayoingiwa na taasisi ili kuiweka taasisi katika eneo salama.
"Ninawahakikishia kuwa serikali itaendelea kutoa msaada wa rasilimali fedha, watumishi, mafunzo, na miongozo ili kuhakikisha kuwa bodi inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa" amesema DC Kalima.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Imani Clemence amewapongeza wajumbe hao kwa kuteuliwa huku akiwasisitiza kuwa mabalozi wazuri wa hospitali katika jamii na kuishauri menejimenti ya Hospitali ya Bombo na kuhakikisha wanafanya uboreshaji kwa kutoa huduma bora.
Pia, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri Dkt. Joseph Mberesero amemshukuru Waziri wa Afya kwa kuwateua na kuwawezesha kupata mafunzo ya kiuongozi ambayo yamewawezesha kuelewa kwa kina majukumu yao huku akiahidi kushirikiana na uongozi wa hospitali kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wagonjwa, miundombinu na usimamizi wa rasilimali.
Mganga Mfawidhi Dkt. Frank Shega amesema “Tunapenda kutoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu kutolewa fedha kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa Hospitali.