Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

AFISA LISHE HOSPITALI YA RUFAA YA BOMBO AELEZA CHANZO CHA UTAPIAMLO KWA WATOTO

Posted on: January 26th, 2024

Na Oscar Assenga,TANGA


Afisa Lishe Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo Mariam Mwakasala amesema tatizo la utapiamlo kwa watoto linaanzia kwa wakina mama  wanaposhindwa kuwanyonyesha kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo.

Mwakasala aliyasema hayo wakati akizungumzia umuhimu wa wakina mama kuwanyonyesha watoto wao maziwa  kwa kipindi cha miezi sita wakati wanapozaliwa kwa ajili ya ukuaji mzuri.

Alisema kwamba wakina mama wanapotoka kujifungua kwa upasuaji au njia ya kawaida wanatoa ushauri kwao kwamba baada ya saa moja ni muhimu kuwanyonyesha watoto bila kuwapa kitu chochote isipokuwa dawa.

“Kwa kweli tunatoa elimu ambayo inakwenda sambamba na elimu ya ulaji bora kwa mama ili aweze kutoa maziwa ya kutosha kwa mtoto kwa sababu changamoto kubwa tunayopata utakuta mama amejifungua mtoto ana afya nzuri tu lakini njia anayomnyonyesha inaweza kusababisha asikue vizuri kwa sababu hamnyonyeshi vizuri kutokana na kutokula vizuri”Alisema

Afisa Lishe huyo alisema mwisho wa siku hali hiyo inasababisha kutokana na mama kutokuwa na maziwa ya kutosha na hatimaye kuanza kumchanganyia na kumpa vyakula ikiwemo uji jambo ambalo linaweza kusababisha utapiamlo kwa mtoto.

“Mwisho wa siku ukiangalia takwimu za wenye utapiamlo zinaanzia kwa mama anaposhindwa kumnyonyesha mtoto vizuri kwa sababu tunapomwambia mama amnyonyeshe kwa kipindi cha miezi sita ya bila kumpa chochote tunategemea ile kwamba mtoto anaweza kunyonya maziwa ya mama na utumbo wake upo tayari kusaga maziwa ya mama tu”Alisema

Alisema ndio maana hawashauri kuwapa watoto maziwa ya kopo ingawa yanakaribiana na virutubisho vinavyopatikana kwenye maziwa ya mama ikiwemo kutoa ushauri kwa wakina mama wahakikisha wanakula vizuri ili waweze kupata maziwa ya kutosha.

Akizungumzia suala Hilo mkazi wa Jiji la Tanga Omari Fundi alisema Kuna umuhimu mkubwa wa wakina mama wajawazito wakawa wanapewa elimu ya umuhimu wa kuwanyonyesha watoto wao pindi wanapozaliwa ili waweze kulia vizuri .

"Lakini pia ni muhimu Sana wakawanyonyesha maziwa watoto kwa kipindi cha miezi sita kwani hapo ndipo wakati muhimu wa watoto kukua"Alisema Omari.