TUGHE TAWI LA BOMBO YAKABIDHI VYETI VYA HESHIMA KWA WANACHAMA WAKE WASTAAFU.
Posted on: July 25th, 2025
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) tawi la Bombo wamefanya sherehe ya kuwaaga waliokuwa wanachama wake kabla ya kuisha muda wao wa kiutumishi.
Hafla hiyo imefanyika leo Julai 25,2025 (jana) katika Ukumbi wa Chuo cha Afya Bombo iliyoongozwa na Mgeni rasmi Dkt. Abdi Msangi Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga pamoja na wanachama wa TUGHE hospitali hapa.
Katika hafla hiyo wanachama wa TUGHE waliandaa zawadi mbalimbali pamoja na vyeti vya heshima kwa wanachama wao kwa utumishi wao uliotukuka.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo pamoja na vyeti kwa Watumishi wastaafu kutoka kada mbalimbali Kaimu Mganga Mfawidhi amewashukuru na kuwapongeza wastaafu hao kwa kufikia hatua hiyo pamoja na kuwatakia kila la heri katika maisha yao nje ya utumishi.
"Niwashukuru na kuwapongeza wastaafu wetu kwa hatua hii kubwa mliyofikia na sisi kama Hospitali tutaendelea kushirikiana nanyi katika hali zote na tunawatakia kila la heri katika kuuanza mwanzo mpya wa maisha yenu nje ya taasisi yetu".
Aidha, Katibu wa TUGHE tawi la Bombo Bi. Enna Msumi ametumia fursa hiyo kuwahamasisha watumishi ambao hawajajiunga na Chama hicho kujiunga ili kuwa kwenye mwamvuli mmoja katika kutetea haki na maslahi yao wawapo katika utumishi.