Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

MKUU WA MKOA TANGA ATOA PONGEZI KWA BOMBO KWA KUFANIKISHA UPASUAJI WA UVIMBE WA KILO 3.5.

Posted on: August 21st, 2026

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani, amepongeza Uongozi na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo kwa weledi na umahiri uliopelekea kufanikisha upasuaji wa kuondoa uvimbe mkubwa wenye uzito wa kilo tatu na nusu uliokuwa ukimsumbua mwanamke mwenye umri wa miaka 38.


Upasuaji huo ulifanyika mwanzoni mwa wiki hii, ambapo jopo la wataalam wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo lilifanikiwa kuondoa uvimbe huo uliokuwa ndani ya kizazi cha mwanamke huyo, aliyekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo kwa muda mrefu.


Dkt. Batilda alitoa pongezi hizo Agosti 20, 2026, wakati alipofika katika Ofisi ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, kabla ya kuelekea kuwafariji na kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya gari iliyotokea wilayani Lushoto.


Amesema mafanikio hayo ni sehemu ya jitihada za wataalam wa afya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kibingwa kwa wakati, na kuwataka watumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa juhudi, weledi na kujituma.


Kwa mujibu wa jopo la wataalam waliohusika katika upasuaji huo, mwanamke huyo hajawahi kupata mtoto na kwamba uvimbe wa aina hiyo unaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazoweza kuathiri uwezo wa mwanamke kupata ujauzito.


Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kibingwa, ikiwemo huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu kwa watu wenye changamoto za ugumba na utasa.