Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

AISHUKURU BOMBO KWA KUMREJESHEA AFYA YAKE NA AFYA YA MTOTO WAKE BAADA YA AJALI YA LUSHOTO.

Posted on: August 28th, 2026

Zainabu Said, mkazi wa Lushoto Mkoani Tanga, ameishukuru Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo kwa huduma na matibabu yaliyomwezesha kurejea katika hali nzuri ya afya pamoja na mtoto wake baada ya kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea Agosti 18, 2026, wilayani Lushoto.

Zainabu na mtoto wake ni miongoni mwa majeruhi wanane waliolazwa katika Hospitali ya Bombo kwa ajili ya matibabu kufuatia ajali hiyo ambapo alipata majeraha katika eneo la kiuno, huku mtoto wake akivunjika mguu.

Baada ya kupatiwa matibabu na uangalizi wa karibu kutoka kwa wataalam wa afya, hali zao imeimarika na leo, Agosti 28, 2026, wameruhusiwa kutoka hospitalini na kurejea nyumbani.

Mama mzazi wa Zainabu,Zuwena Selemani ameupongeza Uongozi pamoja na Watumishi wa Hospitali ya Bombo kwa kujitolea na huduma walizowapatia hadi afya zao zilipoimarika.

Wametoa shukrani kwa Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani, kwa namna Serikali ilivyowashika mkono majeruhi hao baada ya kutokea kwa ajali hiyo na kuhakikisha wanapata msaada unaohitajika.

Hadi leo, Agosti 28, 2026, jumla ya majeruhi saba kati ya wanane waliolazwa Hospitalini hapa wameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali zao kuimarika, huku majeruhi mmoja akiendelea kupatiwa matibabu na uangalizi wa wataalam wa afya.